Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, ameongoza kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya ya Bukoba kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, ambapo masuala muhimu ya kuboresha mazingira ya biashara na kuhamasisha uwekezaji yamejadiliwa kwa kina.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya Mhe. Erasto Sima, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, alisisitiza umuhimu wa wadau kushirikiana kuboresha mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama,usafi wa mazingira na kuangalia uwezekano wa kufanya biashara masaa 24. Alisema:
“Wilaya ya Bukoba ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika ipasavyo zitachochea uwekezaji na kuongeza ajira. Serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha tunafungua milango zaidi ya maendeleo.”

Kwa upande wake, Mbunge Mhe. Mutasingwa alisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wafanyabiashara kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa Wilaya huku akiahidi kusimamia mikopo ya wafanyabiashara wadogo kwa kushirikiana na vyama vyao na benki ya NMB.
Akinukuliwa alisema:
“Baraza hili ni jukwaa muhimu kwa sababu linatupa nafasi ya kusikiliza changamoto zenu na kuona namna ya kuziwekea majibu ya haraka. Lengo letu ni kuhakikisha Bukoba inakuwa kitovu cha biashara na fursa kwa wawekezaji.”
Wadau wa biashara nao hawakusita kutoa maoni yao kuhusu namna ya kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza tija kwenye miradi mikubwa ya kimkakati.
Mwakilishi kutoka SHIUMA Bukoba, Bi. Husna Mohamed Abdallah, ambaye ni Katibu wa SHIUMA Mkoa wa Kagera, alisema:
“Tunapongeza juhudi za Serikali kutusikiliza. Changamoto nyingi za wafanyabiashara zinaweza kutatuliwa kwa mawasiliano ya moja kwa moja kama haya. Tunaona mwanga mpya wa ushirikiano.”
Naye mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania – Bukoba (JWT), Bw. Nicholaus J. Basimaki, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Kagera, alisisitiza umuhimu wa kupunguza urasimu ili kuvutia zaidi wawekezaji. Alisema:
“Urahisishaji wa taratibu za vibali na leseni ni jambo muhimu. Tukipunguza urasimu, hakika idadi ya wawekezaji itaongezeka na pato la wilaya litakuwa kubwa zaidi.”

Kikao hicho kiliangazia pia fursa za uwekezaji katika miradi mikubwa, ikiwemo sekta ya kilimo, utalii, viwanda vidogo na biashara za kimkakati zinazolenga kuinua uchumi wa Wilaya ya Bukoba.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhe. Johnston J. Mutasingwa; Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Bukoba; pamoja na wadau mbalimbali wa biashara kutoka taasisi na jumuiya tofauti zikiwemo TCCIA, Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania – Bukoba, na SHIUMA Bukoba.
Bujunangoma
Anuani ya Posta: P.O.Box 491 Bukoba - Kagera
Simu ya Mezani: 028-2220287
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@bukobadc.go.tz
Hati Miliki 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.Haki zote zimehifadhiwa.