Na.Abel Shema,Bukoba
Hayo yamesemwa katika kikao maalum cha kuwasilisha mipango mikakati ya kupunguza udumavu kutoka katika Halmashauri zote 8 za Mkoa wa Kagera, kilichofanyika Agosti 14,2025 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Akizungumza katika kikao hicho kaimu katibu tawala mkoa wa Kagera Ndugu,Bwai Biseko alieleza mpango huu ni wa miaka 3 ukiwa na lengo la kupunguza tatizo la udumavu katika mkoa wa Kagera kutoka asilimia 34.3 mpaka asilimia 25 kufikia mwaka 2028.
Mpango huu unakuja kufuatia uwepo wa kiwango cha juu cha udumavu mkoani Kagera kwa asilimia 34.3 huku kukiwa na hali ya ukondefu kwa watoto, watoto kuwa chini ya uzito pale wanapozaliwa na upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka 5.
Mikakati hii itaangazia masuala ya udumavu na lishe kwa watu wote na kuleta matokeo chanya kwa Wanawake,Wanaume na Watoto kufikia mwaka 2028.
Katika kuhakikisha hilo linatendeka Halmashauri zote zimekuja na na mipango mikakati kuongeza wigo wa kutoa elimu ya lishe hadi ngazi za vitongoji na vijiji, kushirikisha jamii katika maeneo yenye changamoto,kuhusisha sekta binafsi, kuongeza uzalishaji wa mbegu zilizorutubishwa kama maharage,mchele, kusaga unga ulioongezwa virutubisho na kuhamasisha jamii kutumia teknolojia katika uzalishaji kupitia kilimo cha umwagiliaji,bustani ndogo ndogo na ufugaji wa kisasa.
Wadau mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mpango huu ikiwemo Serikali kupitia TAMISEMI na Wizara ya Afya, kata na Vijiji, Jamii pamoja na sekta binafsi.
Kikao hiki kimehudhuriwa na Kaimu katibu tawala mkoa wa Kagera,Menejimenti ya Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, mganga mkuu wa Mkoa, waganga wakuu wa Wilaya,Maafisa elimu sekondari na msingi,maafisa lishe,pamoja na maafisa mipango.
Mkoa wa Kagera kulinga na sensa ya mwaka 2022 ina wakazi wapatao 2,989,299 wanaoishi katika Wilaya za Biharamulo, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba,Manispaa ya Bukoba, Karagwe,Muleba,Ngara,Kyerwa na Misenyi.
Bujunangoma
Anuani ya Posta: P.O.Box 491 Bukoba - Kagera
Simu ya Mezani: 028-2220287
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@bukobadc.go.tz
Hati Miliki 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.Haki zote zimehifadhiwa.