Na Abel Shema
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh. Erasto Sima amefungua mafunzo ya kamati elekezi na kamati ya wataalam ya maafa ya Wilaya.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Julai, 21,2025.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh.Sima alieleza kamati elekezi na kamati za wataalam zina jukumu kubwa sana la kuratibu na kushughulikia suala la maafa Wilayani Bukoba.
Sima alieleza maafa wakati mwingine hayapigi hodi, elimu ya leo itakua muhimu sana kwa sababu wakati mwingine majanga yakitokea tumekua tukiulizana tunaanza kuyashughulikia vipi haswa ikizingatiwa Wilaya yetu imekua ikikikumbwa na majanga ya mafuriko,tetemeko,upepo mkali pamoja na radi.
‘’Miezi mitatu iliyopita tulipata mvua ya upepo watu walipoteza maisha na kuharibikiwa na mazao yao katika kata ya Kishanje, tulikabiliana na majanga hayo kwa uzoefu lakini sasa tutapata mafunzo na muongozo sahihi wa kujikinga ,kukabiliana,na kurejesha hali za maisha ya awali kwa waathirika wa majanga ‘’ alisema Sima.
Nae mwezeshaji kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Winniefrida Ngowi alieleza lengo la Serikali ni kuhakikisha kamati za maafa za Wilaya zinajiandaa kikamilifu na kuchukua hatua stahiki za kuzuia majanga yanayoepukika na kuandaa mipango madhubuti ya kukabiliana na majanga ya asili kama tetemeko na mafuriko.
Bi.Ngowi aliongeza kuwa mafunzo haya yatajikita Zaidi katika kutambua majukumu ya kamati ya elekezi ya maafa pamoja na majukumu ya kamati ya wataalam katika kukabiliana na maafa.
Nae mwakilishi wa shirika la World Vision Bi. Jackline Kaihula alisema shirika hilo limejikita katika kuhakikisha jamii na kaya zinaweza kujikimu kwa kipato kwa kuwapatia mikopo ya kuanzisha na kukuza biashara ili hata wanapopata majanga wanaweza kuamka tena.
Mafunzo haya yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Kushirikiana na shirika la World Vision na kuhudhuriwa na kamati ya usalama ya Wilaya pamoja na menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.
Bujunangoma
Anuani ya Posta: P.O.Box 491 Bukoba - Kagera
Simu ya Mezani: 028-2220287
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@bukobadc.go.tz
Hati Miliki 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.Haki zote zimehifadhiwa.