WAJAWAZITO KUNYWENI KWA USAHIHI DAWA MPEWAZO KLINIKI
Afisa Lishe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera Bibi Victoria Ngatunga amewasihi wadau wa Afya na Lishe wa Halmashauri ya Wilaya Bukoba kusisitiza matumizi ya dawa za Asidi ya Foliki na Madini ya Chuma zitolewazo kliniki kwa wajawazito ili kusaidia uumbikaji mkamilifu wa viungo vya mwili wa mtoto awapo tumboni.
Bibi Victoria ameyasema hayo leo katika Kikao cha Kamati ya Lishe cha Halmashauri ya Wilaya Bukoba kilichofanyika katika Ukumbi wa Kamati wa Halmashauri ya Wilaya Bukoba ambapo pia amesisitiza wajawazito kuanza mapema kuhudhuria kliniki mara tu baada ya kugundua kwamba ni wajawazito ili waweze kupata huduma stahiki kwa ajili yao na watoto waliomo tumboni.
Katika kuelezea madhara yanayoweza kusababishwa na wajawazito kutotumia dawa za Asidi ya Foliki na Madini ya Chuma, Bibi Victoria alieleza mifano ya vichanga watatu ambao mwanzoni mwa mwaka huu walifikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kagera wakiwa na mapungufu katika viungo vyao vya mwili ambapo kichanga mmoja alizaliwa bila macho kabisa, mwingine alikuwa na tumbo wazi na mwingine alikuwa na mgongo wazi.
Mifano hii hai iliwagusa sana wadau wa Afya na Lishe waliokuwa wamehudhuria kikao hicho na wakaazimu kuendelea kuwahamasisha wajawazito kutumia dawa za Asidi ya Foliki na Madini ya Chuma kwa usahihi huku wakiwaonesha shuhuda za vizazi vilivyoathirika kwa kutotumia dawa hizo kikamilifu na kuwasihi wanaume wawahimize wake zao kuhudhuria kliniki na kuhakikisha wanakunywa dawa wanazopewa huko kliniki.
Naye Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya Bukoba ndugu Desidery Karugaba akasema tafiti za hivi karibuni zinaonesha kwamba asilimia arobaini na nne tu (44%) ya wajawazito nchini ndio hutumia kikamilifu dawa za Asidi ya Foliki na Madini ya Chuma huku wasiotumia wakilalamikia ladha mbaya ya dawa hizo na kichefuchefu kuwa chanzo kikubwa cha wao kutozitumia. Hivyo basi ili kuepuka hilo wajawazito wameshauriwa kunywa dawa hizo wakati wa usiku kabla ya kulala badala ya asubuhi.
Mapendekezo mengine yaliyotewa na Kamati hiyo ya Lishe ni pamoja na shule za Msingi na Sekondari kuendelea kutengeneza bustani za jikoni ili kusaidia wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo jinsi ya kulima bustani za mbogamboga, Idara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii kuhimiza wananchi kutumia kwa chakula mazao wanayoyazalisha badala ya kuzalisha kwa ajili ya kuuza na kupata faida huku afya za familia zao zikizorota.
MWISHO
Pichani ni baadhi ya Wakuu wa Idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya Bukoba wakiwa katika Kikao cha Lishe cha Halmashauri hiyo.
Hawa ni baadhi ya wadau wa afya lishe waliohudhuria katika kikao cha Kamati ya Lishe cha Halmashauri ya Wilaya Bukoba leo
Eneo la Kemondo (Mubembe S/M)
Anuani ya Posta: P.O.Box 491 Bukoba - Kagera
Simu ya Mezani: 028-2220287
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@bukobadc.go.tz
Hati Miliki 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.Haki zote zimehifadhiwa.